makala hii iliandikwa nami katika gazeti la Fahamu. kujibu makala ya Saiboko yenye kichwa cha habari Jee maulid ni uzushi?
Kwa kipindi sasa Jamii za waislamu zimegubikwa na mtafaruku mkubwa sana na usiotarajiwa kumalizika baina ya waislamu wenyewe. mtafaruku huo umechochewa na mambo madogo madogo ya kimtazamo yenye khitalifu ambayo yameunda uaduwi mkubwa, hatimaye kususiana katika harakati mbali mbali, kuitana majina ya ajabu na baadhi ya wakati kutengana katika sehemu za ibada (misikitini). kwa mfano kuna khitilafu baina ya wanaopinga kusoma hitima na wale wanaokubali, khitilafu nyengine ni ya kuaandama kwa mwezi, kadhalika kuadhimisha mazazi ya mtume (maulid).
Wakati waislamu wakikhitalifiana namna hiyo kumekuwa na matatizo tele wa tele yanawakabili katika nyanja zote za kimaisha kisiasa, kiuchumi na hata kijamii. Na wale wasio waislamu kwa upande wao ambao kwa namna moja ama nyengine wanahusika katika kupandikiza mtafaruku huo, sasa wamekaa pembeni wakichekelea kwa magego kwani kwa upande wao kiasi fulani mambo yanamekuwa shuwari katika kiimani na hasa mambo ya kidunia.
Katika gazeti hili toleo na.127, Jumatatu, Aprili 16-22, kwenye ukurasa wa 10, kulikuwa na makala iliyobeba kichwa cha habari kinachosomeka. ‘Jee maulidi ni uzushi?’ Kwangu mimi na mwengine yeyote mwenye mtazamo wa kina na mapenzi ya dhati juu ya dini hii, tusingetegemea kabisa muulizaji wa kiislamu tena msomi kuuliza swali kama hili, kwani sio muafaka kutokana na hali ya waislamu ilivyo sasa, suali hilo linazidisha zile kikhitilafu ambazo huendelza mipaka daima miongoni mwa waislamu.
Lakini kwa kuwa suali limeulizwa, muulizaji alitegemea kubata jawabu, jawabu hiyo huwenda ikawa nzuri au mbaya inategemea na muulizaji suala hilo alivyokusudia kupata jawabu. kama inavyokuwa kwa mwalimu pale anapowatahini wanafunzi wake,baadhi ya wakati hata ikiwa jawabu sahihi lakini mwalimu akisema siyo sahihi hubaki kuwa hivyo hivyo, kwani mwalimu mwenyewe ndiye aliekwishapanga jawabu iwe vipi, na hatimaye mwanafunzi hupata alama ya siyo (wrong) na kupewa alama ndogo au akambulia sufuri kabisa ikategemea na mwalimu mwenyewe, kwasababu hakutimiza matakwa ya swali la mwalimu. Hivyo nakuomba muulizaji na msomaji mwengine yeyote wa makala yangu ambaye anataka kufahamu juu ya swala hili kuwa makini juu ya jawabu niliyoiandaa katika kujibu suali hii, na ningependa pasiwe na mtazamo huo wa mwalimu.
Katika suali hili kuna maneno mawili makuu yaliobeba maudhui ya suali lote yanii maulid (mazazi) na uzushi (bida’ah). Maulidi kilugha (literal) ni mazazi, kisheria (technical) maulid ni sherehe maalum zinayofanywa kila mwaka na baadhi ya waislamu kwa ajili ya kuadhimisha mazazi ya mtume wao Muhammad (s.a.w), kwa kingereza inaweza kuitwa commemoration of Prophet’s Birth day.
Ama uzushi (Bid'ah) katika lugha ni kila kitu ambacho kimeanzishwa si katika mfano ule wa mwanzo, sawa kama ni mzuri au mbaya. Bid'ah katika istilahi ya kisheria ya kiislamu ina maana ya njia, jambo, ibada iliyoanzishwa katika dini, inayoshabihiana na ile njia ya kisheria (lakini kwa hakika si hivyo, yaani inakwenda kinyume na sheria), hivyo wanaozua bid'ah kwa kusudi ya kuwa na ada ya kujikurubisha kwa Allah Aliyetukuka (hii ni kuwa haiwatoshelezi yale yaliyokuja katika sheria na hivyo wanataka kuongeza juu yake kama kwamba wanakamilisha yaliyopungua)”.
(Imaam Abu Ishaaq ash-Shaatiby, al-I’tisaam, Mj.1, uk.37).
Kwa mujibu ya maulamaa wa kiisalmu Bid’ah wamegawanya katika makundi tofauti miongoni mwa hayo ni; Uzushi katika mambo ya kawaida kwa kuzua katika vitu vya kisasa na hii inaruhusiwa kwani asli (msingi) wa mambo haya ni kuruhusiwa. Pili Uzushi katika dini na hapa ndipo zinapoanza khitilafu.
Bid’ah pia imegawika katika makundi mengine mawili bid'ah ya kauli za kiitikadi kama kauli za Jahmiyah, Mu’tazilah, Khawaarij, Rawaafidh (Mashia), Sufi (makundi ya tariqah za dhikri kama Qaadiriyyah, Shaadhiliya, Dandarawiya, Naqshabandiya n.k.) na makundi mengine yote yanayodaiwa kupotea katika mas-ala ya Itikadi. - Aina ya pili ya bid'ah katika kigawanyo hiki ni; kumuabudu M/Mungu kwa ibada ambayo haipo katika sheria. Na hii ina vigawanyo: kwanza: Jambo ambalo katika asli yake ni ibada. Kama kuzua ibada ambayo haina asili katika sheria kama funga na sikukuu ambazo hazipo katika sheria. Pili: Kuongeza katika ibada ambayo ipo katika sheria kama itazidishwa rakaa ya tano katika Swalah ya adhuhuri au alasiri. Tatu: Ni ile ambayo ina sifa ya kutekelezwa kama ibada ya kisheria lakini ikatekelezwa kwa njia iliyo kinyume na sheria na kigawanyo cha nne katika kundi hili: Kuweka wakati au siku maalumu ya kufanya ibada ambayo ipo katika sheria lakini haikuhusishwa kisheria.
Baadhi ya wanzuoni wengine wamezidi kugawa bid’ah katika sehemu tatu; kwanza Bid’ah nzuri na mbaya, na hii imegawanyika katika sehemu tano, bid'ah ambayo ni waajib, bid'ah inayopendeza, bid'ah iliyo makruhu, bid'ah haramu na bid'ah inayokubalika (mubaah) (Imaam ash-Shaatwiby). Pili Bid'atun-hasanah (bid'ah njema). Na kigawanyo cha mwisho katika aina hii ni Bid'ah zote katika dini ni upotevu (Dkt. Yusuf al-Qaradhawi).
Kwa wale wanaokubali kusherekea mauled bila ya shaka , wao wanaamini kuwa ni Bid’ah lakini Bid'atun-hasanah (bid'ah njema) kama tulivyoona katika vigawanyo hivyo hapo juu. Kwani ndani yake kunapatikanwa haya; Kumkumbuka, Kumhishimu, kumtukuza na Kumsifu Bwana Mtume (s.a.w.): kutii amri ya Allah juu ya jambo hili kama katika Qur-an aya hizi: kufurahi, [Yuunus:58]: kumswalia mtume [Al-Ahzaab:56]:
Hoja nyengeine Kwamba Mtume alikuwa akifunga siku ya Jumatatu ambayo ilikuwa siku ya kuzaliwa kwake [hadith ; Imaam Muslim]. Vile vile Katika mkusanyiko wa mauled kuna Kutoleana waadhi, Kujumuika na kushikamana, Kutembeleana na kukirimiana: mbali ya kuwa bid’ah nzuri lakini Wanaongeza kuwa kitendo cha kucheza dufu katika maulid kinadalili pale Maswahaba walimpokea Mtume alipoingia Madiynah kwa Qaswiydah na wengine walikuwa wakimsomea mashairi na kumsifu na yeye hakuwakataza.
Hivyo kwao wao kusherekea mauled siyo jambo baya (uzushi usiofaa), kwani hufanya hivyo ili iwe kumbukumbu kwa watu, na vizazi vyengine pia vipate kumtambua Mtume kwa sherehe kama hizo, pia wanahoji kuwa kutoka na ukweli kuna baadhi ya mambo yamefanyika baada ya kufa kwa Mtume na mengine yanaendelea kufanyika Kama msahafu ulikuwa hauna irabu/harakaat (vokali), au kutumia vifaaa vya kisasa katika dini mfano kipaza sauti (speakers) katika adhaan, kutumia radio, televisheni, mtandao, tovuti, CD's, kupanda magari na kadhalika. kufanya twawaaf juu badala ya chini,. Kwa mujibu ya wanamaulid hawa kama mauled bid’ah na kutumia vitu hivyo pia itakuwa bid'ah.
Kwa wale wanaosema maulid ni haramu kabisa (Bid’ah mbaya) kwa kuwa Dini imekamilika hakuna tena haja ya kuleta jipya ya katika ibada kama maulidi kwani : kuweka ada ya kusoma maulidi ni kuigiza Wakristo (Manaswara) walioweka siku ya Krismasi, Kwenye sherehe za maulidi hufanywa baadhi ya mambo ambayo ni ya munkar (yanayochukiza) kama vile Kuchanganyika kwa wanawake na wanaume, vile vile wanaamini kuwa Hakuna ushahidi wowote wa wazi wa Qur'ani wala Hadithi za Mtume Muhammad, unaothibitisha usawa wa kuyasoma maulidi, kilichokuwemo nimkumfuata na sio kumsifu na mtume mwenyewe amekataza kusifiwa.
Hoja nyengine wanazozitumia wapinga maulidi ni; yamezushwa karne ya nne (miaka mia nne) baada ya kufa Mtume na watu wenye kufru: Makafiri wanafurahi Waislamu wanapofanya Bid'ah kwani ni kuacha mafunzo sahihi ya dini na ni kuzifuta Sunnah za Mtume : Aidha wametoa sababu kuwa Baadhi ya maneno katika Maulidi yana kufru ya kumpandisha Mtume cheo cha usawa na M/Mungu wakati yeye (mtume) amewaonya kufanya hivyo: Nyengine ni pale wasoma mauled wanapoinuka kumswalia Mtume wanaamini kwamba roho yake inahudhuria wakati huo.
Hivyo kwa mujibu wa wanaharakati hao mauled kwao ni haramu kwani hayakuwako au hayakusomwa zama za Mtume Muhammad, maswahaba wala waandamizi wao (taabi'in). kama kweli yangelikuwa ni sawa kuyasoma, bila shaka wangeanza kusoma hao na wangelikuwa ni wa mbele kufanya hivyo, Kwa hivyo, kuyaleta baada yeo ni bid'a (uzushi). Na kila bid'a, kwa maneno yake mwenyewe Bwana Mtume (s.a.w.), ni upotevu. Kwa hivyo, kwa mujibu ya kundi hili kila anayesoma maulidi amepotea na kusisitiza kuwa ni vyema Kuacha mambo yenye shaka na kubakia katika yaliyo wazi:
Hayo ndio malumbano ya hoja baina ya waislamu wenyewe kwa wenyewe katika dhama hizi tulizonazo, kama utajaribu kukaa na kuumiza kichwa juu ya pande zote hizi mbili unaweza kuibuka na maswali mengi sana. kwa mfano wale wanaokubali mauled unaweza kuhoji hivo kwanini usherehekeaji huo mauled umeanza zamani lakini mabadiliko katika jamii bado hayajapatikana? Vile vile kuna baadhi ya waislamu wanashindwa kufanya harambee katika mambo ya kimaendeleo lakini wanaharambee katika mauled, na hapo unaweza kufunga kwa kusema kuwa ni kweli mauled haramu.
Kwa upande wa wanaopinga aidha unaweza kuhoji kuwa; kwa kuwa njia zinazotumika kusherehekea mauled sizo kama kucheza dufu wakati wasala, hivyo maulidi ni haramu. hii sio hoja kamwe kwani uhalali wa kitu hautokani na namna kinavyotendwa ila uasili wake wa kisheria, kwa mfano hatuwezi kuisema elmu ni haramu kwa kuwa wasomi wengi ni walarushwa, ila kinachobakia kuwa haramu ni ule utaratibu wa matumizi ya elimu hiyo, hivyo unaweza kutetea pia mauled siyo haramu ila njia za kusherehekea ndiyo haramu.
Kwa hakika khitilafu ndogo ndogo baina ya waislamu zilikuwepo tangu wakati wa mtume. kisamaarufu kinaeleza kuwa mtume alipeleka jeshi la waislamu kwa mayahudi wa madina ukoo wa Quraidha (banii kuraidha ), na kuwambia kuwa; “musisali sala ya Alaasir ila Ban-Quraidha (sehemu waliyokuwa wakiishi hao mayahudi), wakati maswahaba wanaelekea huko, njioani sala iliwakuta ndipo baadhi yao walisali hapo hapo kwa hoja kuwa ‘sala ni kwa wakati wake’ na kuwa mtume alisema vile kwa ajili ya kuwaharakisha tu, lakini baadhi yao hawakusali wakidai kutii amri ya mtume kusali huko Ban-Quradh. Wakati wa kurudi kila mmoja alikuwa na hamu ya kumuuliza mtume lakini mtume aliwambia kuwa wote wako sahihi.
Sasa ikiwa mtume mwenyewe ameonesha kuzinyamazia khitilafu ndogo ndogo kama hizi inakuwaje leo hii waislamu wenyewe kwa wenyewe waekeane chuki, majungu, kuitana majina mabaya ( kama wahabi, au bakwata) kwa kuwa wametofautiana kimtazamo.
Ni wazi kuwa viumbe (binaadamu) wote hawako sawa katika kila hali mfano vipaji, rangi, kiuwezo. Hivyo na kimtazamo vile vile vigumu kuwa sawa.Hivyo ni vyema basi kila muislamu kustakimu katika msimamo anouona mwenyewe kuwa sahihi, lakini nisharti muislmau huyo na hoja na dalili za wazi kutokana na elimu sahihi za msimamao huo.
Na kwa wale wanaoamini kusoma maulidi siyo vibaya kwao, nawaomba waitumie nafasi hiyo ya mikusanyiko ya waisalmu kuwa ndiyo chachu ya kuwaweka na kuwahamasisha waislamu katika kuyaendea maendeleo yao ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Nakumbuka mwaka jana katika siku ya sherehe kama hizo pale umoja wa wanafunzi wa kiislamu chuo cha Muhimbili walipoandaa semina elimishi ambayo kila mmoja aliyehudhuria hafla hiyo alirudi na taaluma fulani aliyoipata katika mkusanyiko huo. Nadhani huo utakuwa mfano bora wa kuigwa kwa wale waadhimishaji wa maulidi.
Khamis J. Abdullah
MUM, 2nd year Student,
Mass Commnunication.
Tel. 0714 235040.
chichiboy2006@hotmail.com
2 comments on Mauli, Khitilafu Ndogo, Isiyopasa Kuwagawa Waislam
Add a comment
To add comments without entering your email and image verification, you must be logged in. Login or Join Blogster



[THUMBUP]